News

October 29th, 2012
Picha ni, Mh. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka akimkabidhi Mh. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete anwani ya Ofis
September 21st, 2012
Includes new regions and districts
September 11th, 2012
FINANCIAL YEAR: 2012/2013

Extra Menu

TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU TAMKO LILILOTOLEWA NA ISMAIL JUSSA LADHU WA CHAMA CHA WANANCHI CUF

Submitted by alexkaraba on Fri, 01/27/2012 - 15:51
KUHUSU MRADI WA KUONGEZA ENEO LA ZIADA NJE YA UKANDA WA KIUCHUMI BAHARINI
TANZANIA EXTENDED CONTINETAL SHELF
TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU TAMKO LILILOTOLEWA NA ISMAIL JUSSA LADHU WA CHAMA CHA WANANCHI CUF KUHUSU MRADI WA KUONGEZA ENEO LA ZIADA NJE YA UKANDA WA KIUCHUMI BAHARINI (TANZANIA EXTENDED CONTINETAL SHELF)
1.0             Utangulizi:
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya Serikali ya Muungano wa Tanzania imepokea taarifa ndani ya vyombo vya habari (hususan magazeti ya Nipashe na Guardian ya tarehe 23 Januari, 2012) kuhusu somo tajwa hapo juu kwa mshangao. Wizara imeona ni vyema kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:
Sheria ya Umoja wa Mataifa juu ya Mikataba ya Sheria ya Baharini (The United Nations Convention on the Law of the Sea – UNCLOS) ilianzishwa mwaka 1982  ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliridhia tarehe 30 Septemba 1985. Sheria hii ilianza kutumika rasmi tarehe 16 Novemba, 1994 (Ona tovuti  http://www.un.org/depts/los/clcs_new/submissions_files/submission_tza59_2012.htm).
Baada ya kuridhiwa kwa Sheria hiyo, Baraza la Mawaziri kwa Waraka Na. 38 wa 2008 liliiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutekeleza mambo yafuatayo:-
  1. Iendelee na utekelezaji wa makubaliano ya Kimataifa juu ya Sheria ya Bahari ya mwaka 1985 (The United Nations Convention on the Law of the Sea). Makubaliano hayo ni pamoja na kuainisha mipaka Baharini na nchi jirani.
  2. Iendelee na mchakato wa kudai eneo la nyongeza nje ya ukanda wa kiuchumi Baharini.Mchakato huo ikiwa ni pamoja na kukusanya takwimu za jiolojia na taarifa nyingine ili kuthibitisha iwapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inastahili kudai eneo la nyongeza nje ya ukanda wa kiuchumi Baharini.
2.0 Utekelezaji
Katika kutekeleza majukumu hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alipewa jukumu la kuunda Kamati mbalimbali ambazo zitatekeleza Mradi huu. Kamati zilizoundwa ni pamoja na:
1.      Kamati ya Makatibu Wakuu – Steering Committee
2.      Kamati ya Ufundi – Technical Team
3.      Kamati ya utekelezaji – Technical Core Group
Mara baada ya kuundwa kwa kamati hizi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliomba msaada kutoka Serikali ya Norway katika utekelezaji wa mradi huu. Katika barua ya kuomba msaada, muundo wa Kamati mbalimbali za mradi zimeanishwa zikionyesha majina ya wajumbe na Taasisi wanazotoka wakiwemo wajumbe kutoka Zanzibar. Serikali ya Tanzania iliingia Mkataba na Serikali ya Norway tarehe 17 January 2008 kufadhili utekelezaji wa mradi huu. Mkataba huu ulisainiwa na Bw. Ramadhan M. Khijjah akiwa wakati huo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kazi ya kukusanya takwimu baharini ilifanyika kuanzia mwaka 2008 hadi 2012 na ilifanyika kwa  ushirikiano wa Wizara za NJE, Katiba na Sheria, Wizara ya Nishati na Madini, Chuo kikuu cha Dar es salaam, Institute of Marine Science Zanzibar, Chuo Kikuu Ardhi na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC). Kampuni ya GX Technology ya Marekani ilipewa tenda ya kukusanya takwimu Baharini. Kikosi kazi cha mradi huu (Technical Core Group) kilitumia takwimu zilizokusanywa na Kampuni hii katika kutayarisha Andiko la kudai eneo hilo.
Katika kuhakikisha kuwa Mikataba ya Sheria ya Baharini inatekelezwa, Umoja wa Mataifa ulitoa muda wa hadi kufikia mwezi Mei 2009 kuwa nchi zinazopakana na Bahari ziwe zimewasilisha nia ya kudai eneo la ziada nje ya ukanda wa kiuchumi Baharini. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutambua umuhimu wa kudai eneo hilo, ilipeleka Andiko la awali (Preliminary Information Document- (PID)) na kukubaliwa na Umoja wa Mataifa tarehe 7 Mei, 2009. Andiko la mwisho la kudai eneo la nyongeza nje ya ukanda wa kiuchumi Baharini lilitakiwa kuwa limewakilishwa ifikapo tarehe 13 Mei, 2011 la sivyo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ingelipoteza haki yake. Hata hivo kwa sababu za ukosefu wa fedha, Serikali iliomba kupewa muda zaidi kukamilisha kazi hiyo na hatimaye andikio limewasilishwa Umoja wa Mataifa tarehe 18 Januari 2012. Kinachoendelea sasa ni mchakato wa kutetea andiko hilo katika Tume ya Mkataba wa Sheria ya Baharini.
3.0           Ushiriki wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Ushiriki wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kutekeleza mradi huu ulikuwa mkubwa na muhimu na unaonekana katika wajumbe wa kamati mbalimbali za mradi zilizoundwa tangu mwaka 2007. Wajumbe walioteuliwa katika Kamati mbali mbali ni kama ifuatavyo:-
  1. Kamati ya Makatibu Wakuu (Steering Committee) - Bw. Mwalim A. Mwalim, Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Nishati, Ujenzi na Makazi
  2. Kamati ya Ufundi (Technical Committee) - Bw. Haji Adam Haji aliyekuwa Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ameshiriki kikamilifu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi. Aidha, wakati wa kupima alama za Baseline mwezi Januari 2011 kikosi kazi kutoka Tanzania Bara kilishirikiana na wataalam wapimaji kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kukamilisha kazi hiyo. Upimaji huu ulifanyika chini ya usimamizi wa Masheha wa Kiuyu, Maziwa Ng’ombe, Kojani na Vitongoji kwa upande wa Kisiwa cha Pemba na Makunduchi kwahuu upande wa Kisiwa cha Unguja. Pia Bwa. Omar Zubeir – aliteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati.
  3. Kamati ya Utekelezaji (Technical Core Group) – Bw. Pandu S. Makame kutoka ofisi ya Makamu wa Rais. aliteuliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Kikosi kazi (Technical Core Group) cha mradi huu.
  4. Kuwasilisha Andiko Umoja wa Mataifa: Andiko liliwasilishwa makao makuu ya Umoja wa Mataifa, mjini New York, Marekani, tarehe 18 Januari, 2012. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Prof. Anna Tibaijuka aliongoza ujumbe wa viongozi na wataalam 10 wakiwemo wajumbe 2 kutoka Zanzibar.Mhe Shamhuna, Waziri wa Ardhi, Maliasili na Nishati hakuweza kuhudhuria lakini alimteua ndugu Ayoub Mohamed Mahmoud, Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti katika Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Ujenzi kumwakilisha. Bw. Ayoub Mohamed Mahmoud alishiriki kikamilifu katika ziara hiyo na kupewa nafasi kuongea kwa niaba ya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Aidha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alialikwa kuteua Wabunge wawili katika ziara hiyo ya kihistoria. Mhe. Abdulrahman Hassan Shah, Mbunge wa Mafia aliwakilisha Tanzania Bara na Mhe. Zhakia Hamdani Meghji aliwakilisha Zanzibar.  Bw. Mhamed Juma Omary, Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Zanzibar alishindwa kusafiri dakika za mwisho kwa sababu ya dharura iliyojitokeza hivyo kukatisha safari yake mjini Dar es Salaam.
4.0 Hitimisho
  1. Madai ya Mhe.Ismail Jussa Ladhu wa Chama cha Wananchi CUF kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikushiriki au kushirikishwa katika zoezi hili hayaendani na yaliyojiri. Ukweli ni kwamba wajumbe na viongozi kutoka SMZ wameshiriki na kufanya kazi kwa bidii katika zoezi zima.
  2. Sheria ya Umoja wa Mataiafa ya Mikataba ya Sheria Baharini ulioridhiwa mwaka 1985, ulifanywa kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano. Sheria hiyo inahusu nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na Tanzania Bara na Visiwani, kwa mujibu wa sheria hizo, ni nchi moja. Aidha mipaka yoyote ya nchi baharini au nchi kavu ni kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nchi jirani na si kati ya sehemu yoyote ile ya muungano huo.
  3. Kwa mantiki hiyo, utekelezaji wa Sheria ya Umoja wa Mataiafa ya Mikataba ya Sheria Baharini namba 76, ulifanywa kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.
  4. Vile vile, mipaka ya eneo la kiuchumi Baharini (Exclusive Economic Zone) iliainishwa mwaka 1982 na kuwasilishwa Umoja wa Mataifa kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  5. Mipaka iliyoainishwa Baharini ni ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na isihusishwe na kugawana kwa rasilimali zilizomo ndani ya mipaka hiyo, jambo ambalo linahusu makubaliano ndani ya nchi (internal matter) na halitambuliki katika ngazi za Umoja wa Mataifa. Aidha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi haishughulikii jambo hilo la ugawanaji wa rasilimali ndani ya nchi iwe baharini au nchi kavu. Kwa hiyo si sahihi kuhusisha mgawanyo wa rasilimali zilizomo Baharini  na mchakato wa kudai eneo la nyongeza nje ya ukanda wa kiuchumi Baharini katika uwanja wa kimataifa. Hoja zozote kama zipo zinajadilika ndani ya nchi.
  6. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, katika shughuli zake za kuainisha mipaka, iko tayari kutoa taarifa zaidi kwa wananchi wa Tanzania Bara na Visiwani wanaotaka maelezo zaidi au kuangalia ramani za mipaka ya nchi yetu na mikataba ya kimataifa inayohusika. Ni jambo nyeti linalohitaji utafiti wa kutosha. 
PATRICK RUTABANZIBWA
KATIBU MKUU

  (Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti  http://www.un.org/depts/los/clcs_new/submissions_files/submission_tza59_2012.htm).