News

May 8th, 2012
Application Form
April 16th, 2012
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi yasherehekea miaka 50 ya Uhuru
April 12th, 2012
Mhe. Prof. Anna Tibaijuka (Mgeni rasmi ) katika sherehe hizo

Extra Menu

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Submitted by alexkaraba on Mon, 10/03/2011 - 11:45
Mkutano wa Sekta ya Ardhi
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI
 
 
 
 
 
 

 

 

 
 
 
 
 
HOTUBA YA MGENI RASMI MHE. GOODLUCK OLE – MEDEYE (MB)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI KWENYE UFUNGAJI WA MKUTANO WA SEKTA YA ARDHI UKUMBI WA BLUE PEARL, UBUNGO PLAZA DAR ES SALAAM TAREHE 29 SEPTEMBA, 2011
 
  
 
 
Ndugu Mwenyekiti,
Wahe. Wakuu wa Wilaya mliopo hapa,
Wakuu wa Idara na Taasisi chini ya Wizara,
Wageni waalikwa kutoka Taasisi mbalimbali,
 Ndugu Washiriki,
Wanahabari wote.
Mabibi na Mabwana
 
Ndugu Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetumeweza kufika hapa kushiriki katika mkutano huu muhimu wa Sekta ya Ardhi ambao leo unafikia kilele. Ninaamini kuwa kumalizika kwa mkutano huu ni mwanzo wa kujipanga kwa ajili ya utekelezaji wa maazimio yetu ambayo naamini yamezingatia sera na sheria za sekta yetu.
 
 Ndugu Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kumpongeza Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakuu wa Idara na Taasisi zote zilizo chini ya wizara na watumishi wote kwa kufanikisha maandalizi na uendeshaji wa mkutano huu. Aidha nawapongeza wajumbe wote kwa kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika vikao vilivyofanyika mfululizo kwa muda wa siku nne. Ninaamini kuwa mazingira mazuri ya eneo hili yaliwezesha wajumbe kutoa michango yao ipasavyo.
 
Nimejulishwa kuwa mkutano huu ambao kaulimbiu yake ni ‘Tuzingatie sheria, uweledi na uadilifu kwa huduma bora za ardhi na makazi’ umehudhuriwa na wajumbe wapatao 775. Hii ina maana kuwa idara zote
 
 
za wizara, taasisi zake na wilaya zote nchini zimewakilishwa kikamilifu katika mkutano huu. Vile vile nimejulishwa kuwa wajumbe wote walipata fursa ya kujadili mada zilizowasilishwa na changamoto zilizoibuliwa katika ngazi ya Idara au taasisi na kutoa maazimio kupitia kikao cha majumuisho ya pamoja. Kwa mantiki hiyo maazimio yaliyofikiwa yametokana na maoni na matakwa yenu yaliotolewa bila shinikizo hivyo utekelezaji wake utakuwa rahisi kwa vile ninyi ndiyo watekelezaji katika maeneo yenu ya kazi.
 
Ndugu Mwenyekiti, Changamoto za sekta ya ardhi ni nyingi na si rahisi kuzijadili katika siku nne na kujiridhisha kuwa tumekamilisha uchanganuzi wake kwa kina. Naamini kuwa kwa siku nne tulichofanya ni uchokozi tu ambao utatuwezesha kuibua chnagamoto zaidi katika maeneo yetu ya kazi na kutafuta ufumbuzi mwafaka kwa mazingira hayo. Kila mjumbe hana budi kuwa na nyaraka ambazo atazitumia kama mwongozo wake,  ili ajipime kwa kiasi gani anaondoa au kupunguza changamoto zinazotokana na utendaji wake binafsi au ofisi yake.
 
Katika ufunguzi  wa   mkutano  huu,  Mhe  Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka (Mb) Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya ardhi na nyumba ambazo pia zimeanishwa kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2011/20112. Nimejulishwa kuwa kila mjumbe amepata nakala ya hotuba ya ufunguzi wa mkutano huu. Ili kufanya kurahisisha utayarishaji wa mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizo katika sekta yetu ni vizuri kila mjumbe atakaporudi kwenye kituo chake cha kazi akatoa nakala kwa
 
viongozi wake (kwa wale anaotoka kwenye Halmashauri) na kila mtumishi aliye katika ofisi yake. Kwa pamoja wajadaliane na kuandaa mikakati ya kutekeleza maazimio hayo na watoe taarifa ya utekelezaji kila mwezi.
 
Ndugu Mwenyekiti, nimesikia maazimio mbalimbali yaliyofikiwa katika mkutano huu. Kujadili changamoto na kufikia maazimio ni hatua ya awali tu katika kuondoa changamoto. Hatua ambayo inastahili kuangaliwa kwa makini ni utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa. Hii ndiyo changamoto inayotokana na mkutano huu. Tunapoagana leo uwe mwanzo wa kila afisa na kila Idara kujiwekea vigezo vya namna ya kujipima kuhusu utekelezaji wa maazimio ya mkutano huu.
 
Ndugu Mwenyekiti, Ninawapongeza wajumbe kwa kujituma, uwazi, umahiri na umakini mkubwa waliouonesha katika kuchangia mada. Hoja mbalimbali zilibuliwa na kuwekewa muda wa utekelezaji wake. Ninaagiza Wakuu wa Idara katika Wizara na Halmashauri waweke vipaumbele katika maazimio yao ili iwe rahisi kupanga nyenzo na raslimali watu. Ninaagiza pia kila Idara iandae vigezo vya kisayansi vya kupima utekelezaji wa maazimio au kushughulikia changamoto zilizoibuliwa katika eneo lake.
 
Ndugu Mwenyekiti, nisingependa kuchukua muda mrefu kwani, wajumbe wamekwishapata mengi ya kuyafanyia kazi baada ya kutawanyika jioni hii. Hata hivyo ningependa kusistiza mambo yafuatayo:
 
ØTuache kufanya kazi kwa mazoea. Kwa mfano, kama una jukumu la kukusanya kodi ya pango la ardhi tunapaswa kutoka ofisini na kufuatilia wadaiwa badala ya kusubiri atakayejitokeza alipe,
 
ambaye hatajitokeza basi. Tufanye kazi kwa malengo na kubuni mbinu zitakazotuwezesha kufikia malengo;
 
ØTujifunze kukusanya kuweka na kutumia vyema takwimu na taarifa zilizopo. Tumekuwa wepesi wa kutoa  visingizio kama vile ukosefu wa kompyuta kila tunapokosa taarifa muhimu. Natoa wito kwa maafisa wote kwenye sekta wawe wabunifu kwani ingawa vifaa kama computer ni vitendea kazi muhimu kuwepo kwao ni jambo moja na kutumika kikamilifu ni jambo lingine. Unaweza kuwa na vifaa na bado usitekeleze wajibu wako ipasavyo. Kwa mfano, inakuwaje, mpima mwenye vifaa vya kisasa akapima juu ya ardhi ambayo ytayari imepimwa na kumilikishwa? Anashindwaje kutafuta taarifa za upimaji za kutosha kuhusu upimaji uliopita wa eneo linalohusika?; 
 
ØTuwajali wateja wetu. Kila mmoja wetu anapaswa kutambu kuwa nafasi aliyo nayo imetokana na kuwepo mahitaji ya huduma ya fani yake. Swali la kujiuliza ni kuwa je, wadau wa huduma zetu wana njia mbadala ya kupatia huduma? Au je, ni sisi tu ndiyo wenye ujuzi na uwezo wa kutoa huduma hizo au wapo wengine? Vyo vyote vile jibu liwavyo suala la msingi ni kuwa tumeajiriwa kwa sababu huduma zetu zinahitajika. Hata hivyo wateja wetu wakichoka na tabia zetu watatususia na kufanya waonavyo ili mradi watimize haja zao. Ujenzi holela unatokana na wananchi kuepuka urasimu uliopo katika upangaji na mchakato wa umilikishaji wa ardhi. Vivyo hivyo watu kujichukulia sheria mikononi hutokana na vyombo vya sheria kushindwa kutimiza wajibu wao. Mwisho wa haya yote ni matukio tunayoyaona hivi sasa katika nchi za Kiarabu ambapo wananchi
  
wameamua kuondoa serikali madarakani. Tutimize wajibu wetu kwani ikiwa wananchi watakasirika na kuamua kuchukua madaraka waliotukabidhi watakaoathirika ni ninyi na familia zenu.
 
ØUshirikiano na uadilifu iwe nguzo yetu. Tuepuke tabia ya kuweka mitandao ya kushirikiana katika kukiuka sheria, kanuni na taratibu zisiwepo tena. 
 
ØKuongeza mapato na kupunguza matumizi ya Serikali. Tunapoondoka hapa kila mmoja atafakari kwa namna gani atawezesha Serikali kupata kodi halali ambayo siyo mzigo kwa wananchi na kuhakikisha kuwa kila kodi inayostahili inalipwa yote na kwa wakati. Hata hivyo ukusanyaji wa maduhuli uende sambamba na nidhamu katika matumizi.
 
ØKuthubutu kusimamia Sera, Sheria, Kanuni, Miongozo na taratibu. Kauli mbiu ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru itumike kutuchochea kutekeleza sheria na maelekezo yaliyopo na yatakayotolewa. Ninyi kama wataalamu katika fani zenu hamna budi kutambulika kwa msimamo na mwenendo mwema wa kuzingatia sheria. Msishawishike kwa fedha. Msiogope majaribu au vitisho kutoka kwa wanaotumia nafasi zao za kifedha. Serikali itakulinda kama ukithubutu kutekeleza majukumu yako kwa kuzingatia sheria.
 
Ndugu Mwenyekiti, kama nilivyosema hapo awali leo sitakuwa na mengi ya kusema isipokuwa nina ahadi moja kwa  wajumbe kuanzia leo
 
Mhe. Prof Anna Kajumulo Tibaijuka Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, pamoja na mimi tutakuwa na kazi moja tu kufuatilia kwa karibu uthabiti wa kauli zenu na maazimio yenu. Wananchi wanataka kuona mbadiliko katika matendo na huduma zetu siyo mabadiliko katika maneno au maazimio. Wanataka kuona haki ikitendeka katika sekta hii. Hawapendi kuona Wizara ya Ardhi ikiwa kama tawi la mahakama ya kutatua migogoro ya ardhi.
 
Ninawashukuru tena kwa kufika kwenu katika mkutano huu. Ninaamini kuwa Mijadala iliyofanyika italeta mafanikio katika kuendeleza sekta ya ardhi nchini. Mzingatie michango iliyotolewa na kuitekeleza kwa  uaminifu. Ninaamini maazimio mliojiwekea yataongeza ufanisi na tija katika kutoa  huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia sheria, weledi na uadilifu.
 
Ndugu Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sasa kwa heshima na furaha isiyo kifani natangaza kuwa Mkutano Mkuu wa Sekta ya Ardhi wa Mwaka 2011 umefungwa rasmi. Nawatakia wote safari njema kurudi kwenye vituo vyenu vya kazi. Mwenyezi Mungu apende kuwabariki na kuwajalia moyo wa upendo kwa wananchi mnaowahudumia.
 
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
 
Matukio katika picha