HOTUBA YA MGENI RASMI, MHE. PROF. ANNA KAJUMULO TIBAIJUKA (MB)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO WA SEKTA YA ARDHI
UKUMBI WA BLUE PEARL, UBUNGO PLAZA
DAR ES SALAAM TAREHE 26 SEPTEMBA, 2011
Mhe. Said Mecky Sadiki, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Wahe. Wakuu wa Wilaya za Dar es Salaam mliopo hapa,
Wakuu wa Idara na Taasisi chini ya Wizara,
Wageni waalikwa,
Ndugu Washiriki,
Wanahabari wote.
Mabibi na Mabwana
Ndugu Mwenyekiti
Awali ya yote, napenda kuchukua fursa hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia sote kuwa hapa leo kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano huu wa Sekta ya Ardhi.
Kwa namna ya pekee nawashukuru wageni waalikwa wote kwa kufika kwenu; nafahamu mna majukumu mengi lakini mmekubali kuwa nasi hapa leo. Nawapongeza sana.
Pili, Nampongeza Mhe. Naibu Waziri kwa kazi nzuri anazofanya. Vile vile nawapongeza Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kwa maandalizi mazuri ya Mkutano huu.
Tatu, Napenda kuwapeni pole kwa uchovu wa safari ndefu washiriki wote mnaotoka Mikoani. Nina imani kuwa madhari nzuri na hali ya hewa ya hapa mlipo imewaburudisha na kuwaondolea uchovu. Kwa mantiki hiyo ni imani yangu kuwa ushiriki wenu utakuwa mzuri na wenye kuleta tija katika Sekta ya Ardhi.
Nilifarijika nilipoelezwa kuwa mkutano huu unawashirikisha watendaji kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na, Halmashauri za Majiji, Miji, Wilaya na Sekretarieti za Mikoa nchi nzima. Aidha nimefurahi zaidi kwa kuwepo waalikwa kutoka Sekta binafsi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) wanaojishughulisha na masuala ya uendelezaji wa ardhi. Asante sana na karibuni. Lakini nimefurahi zaidi baada kuambiwa kuwa asilimia 60 ya wajumbe ni wawakilishi kutoka Halmashauri mbalimbali hapa nchini. Huu ni utaratibu mzuri kwa sababu masuala yote ya ardhi yako kwenu.
Ndugu Mwenyekiti, Nimeambiwa kuwa kwa mara ya mwisho mkutano kama huu ulifanyika mwaka 2006. Ni takribani miaka mitano ambapo ni muda mrefu na kuna mabadiliko mengi yaliyotokea tangu wakati huo, kwa hiyo tunayo kila sababu ya kukutana leo.
Ndugu Mwenyekiti, Nakupongeza sana kwa kauli mbiu ya mwaka huu ya ‘Tuzingatie Sheria, Uweledi, Uadilifu kwa huduma bora za Ardhi na Makazi’ambayo inaenda sambamba na Kauli mbiu ya miaka 50 ya Uhuru. Kwa kuwa wengi wenu ni wazoefu katika sekta hii ya ardhi mnafahamu kwa nini kauli mbiu hii imechaguliwa. Vile vile mnafahamu vizuri kuwa taswira ya sekta ya ardhi miongoni mwa jamii yetu na wageni siyo ya kuridhisha sana. Sekta hii kama inavyojulikana kama Sekta Mtambuka ni Sekta iliyojaa changamoto nyingi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya kitaalam.
· Ndugu Mwenyekiti, Mkutano huu unalenga kujipanga katika kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoikabili sekata hii. Hivyo basi tutumie fursa hii kujipanga ili kubadili taswira mbaya iliyojengeka katika sekta hii. Aidha, napendekeza tujipange katika maeneo yafuatayo:-
· Tujipange ili kuifanya ardhi kuwa mtaji wa kweli kwa mwananchi na wadau.
· Tujipange ili kuifanya sekta ya ardhi kuwa mojawapo ya njia kuu za uchumi kitaifa.
· Tujipange ili kubadili muonekano wetu miongoni mwa jamii, tusijulikane tena kama ‘mafisadi wa ardhi’.
Ndugu Mwenyekiti, Mimi pamoja na Naibu Waziri, Mhe. Goodluck Ole Medeye (Mb.), hatujamaliza mwaka mmoja katika Wizara hii. Lakini katika kipindi hiki kifupi tumejifunza mambo mengi kutoka kwenye sekta hii yakiwemo mengi ya kujivunia. Vile vile tumejifunza kuwa sekta hii inaongozwa kwa kutumia sheria na utaalamu wa hali ya juu. Lakini pia tumeona changamoto nyingi, baadhi yake zinaitia aibu sekta hii kwa kutupaka matope wote tuliomo ndani yake ingawa zinasababishwa na wachache miongoni mwetu. Hawa ni wale wanaongozwa na malengo binafsi badala ya kuongozwa na Sheria, kanuni na taratibu za kiutendaji. Napenda niwakumbushe baadhi ya changamoto za kiutendaji zilizopo katika sekta hii na ambazo zinakwamisha utendaji:
(a) Utoaji wa huduma kwa wateja ulio chini ya kiwango na matarajio ya wanaopewa huduma hizo.
(b) Ukusanyaji hafifu wa maduhuli ya serikali,
(c) Ukiukaji wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo.
(d) Kutozingatia utaalamu na miiko ya taaluma
(e) Ukosefu wa kumbukumbu sahihi za ardhi na makazi n.k.
Ndugu washiriki wa mkutano ni matumaini yangu kuwa kila mmoja wenu atatumia vizuri fursa ya mkutano huu kujitathmini, Kujichunguza na kujibainisha binafsi na kitaasisi kwa kiasi gani anachangia kupunguza au kuongeza changamoto hizo. Ninapenda majadiliano mtakayoyafanya katika vikao vyetu yajikite katika kutafuta vyanzo na ufumbuzi wa changamoto hizo.
Ndugu Mwenyekiti, Mtakumbuka kuwa hivi karibuni Bunge la Bajeti la mwaka 2011/2012 limemaliza kikao chake. Kwa wale mnaofuatilia mambo, mtakumbuka kuwa kuna masuala yalitojitokeza kutoka kwa Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi kuwa ni kwa kiasi Watanzania wanataka mabadiliko katika sekta hii. Ni dhahiri kuwa Watanzania wanataka huduma bora, hawataki migogoro ya ardhi. Wanachukia huduma zilizo chini ya kiwango, wanataka kufaidika na ardhi yao pale inapotwaliwa kwa matumizi ya serikali au uwekezaji wa aina yoyote na pia wanakiu ya mabadiliko katika Sekta ya hii.
Pia, Katika hotuba yangu ya Bajeti niliyoiwasilisha tarehe 15 - 16 Agosti 2011 nilitoa changamoto saba zinazoikabili sekta ya ardhi ambazo nataka Wajumbe wote mzielewe mzitumie katika kuongoza majadiliano yetu. Na hapa napenda nizitaje kama ifuatavyo:-
(i) Mifumo mibovu ya utunzaji wa kumbukumbu za Sekta ya Ardhi;
(ii) Ardhi kwa ajili ya uwekezaji na matumizi mbalimbali ya Serikali kutopatikana kwa urahisi mijini na vijijini;
(iii) Uelewa mdogo wa wananchi, viongozi na watendaji wengi kuhusu sera, sheria na kanuni za uendelezaji ardhi, nyumba na makazi;
(iv) Gharama kubwa za utayarishaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, upangaji wa miji na upimaji wa ardhi. Upungufu mkubwa wa nyumba bora mijini na vijijini na riba kubwa ya mikopo ya nyumba inayotolewa na taasisi za kifedha (mabenki);
(v) Ujenzi holela mijini na uvamizi wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya huduma za jamii kama vile maeneo ya wazi;
(vi) Kuongezeka kwa migogoro ya ardhi na nyumba hasa kwa maeneo ya mijini na vijijini; na
(vii) Nakisi ya bajeti inayotengewa Sekta ya Ardhi
Ndugu Mwenyekiti, ikumbukwe kuwa fedha ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa ahadi zetu. Ninapenda mtafakari mikakati itakayowezesha upatikanaji wa maduhuli na kuvuka lengo tulilojiwekea la kukusanya shilingi bilioni 20.665. Uvukaji wa malengo ya ukusanyaji wa maduhuli utawezesha utekelezaji mzuri wa malengo yetu. Utawezesha pia kuweka mazingira mazuri ya kazi katika ofisi zitakazokusanya zaidi. Napenda kuwaletea habari njema kwamba kuanzia mwaka huu wa fedha marejesho ya makusanyo yatakuwa asilimia 30 badala ya asilimia 20 mlizokuwa mnapata. Kwa hiyo Halmashuri zitakazokusanya zaidi zitanufaika zaidi. Pia Halmashauri zitakazoshindwa kufikia malengo yao zitawajibishwa.
Ndugu Mwenyekiti, Pia, katika hotuba yangu ya bajeti 2011/2012 niliorodhesha majukumu kumi na tatu ambayo Wizara hii imejipangia katika kukabiliana na changamoto nilizozitaja. Nataka nizungumzie majukumu matatu tu ambayo ni ya kuhamasisha na kuiweka jamii ya watanzania na wadau kufaidi matunda ya Sekta ya Ardhi. Majukumu hayo ni:-
(a) Kutoa elimu kwa umma na kwa viongozi na Watendaji wa Serikali za Mitaa kuhusu Sera, Sheria na kanuni za Ardhi, Nyumba na Makazi nchini. Hili ni jukumu ambalo hakuna hata mmoja wetu anaweza kulikwepa kuanzia Wizara hadi Mamlaka za Mijini na Wilaya. Kila mtu anawajibika kuzielewa Sheria na Kanuni za ardhi popote alipo kazini au nje ya kazi kwa kadiri ya uwezo wake na kutoa ushauri stahiki kwa Serikali kupitia viongozi wake. Kwa masikitiko makubwa napenda kutamka kuwa kwenye ofisi zetu kuna udhaifu mkubwa katika utekelezaji wa sheria hizi. Watumishi wa Sekta hii wasio waadilifu wamekuwa wakiziyumbisha sheria na kanuni hizi kwa makusudi. Napenda niseme hapa leo kuwa waliozoea tabia hiyo, hatuna nafasi kwa ajili yao tena. Wajiondoe kabla hawajaondolewa.
(b) Kuimarisha jukumu ya kusimamia maendeleo ya ardhi mijini: Ndugu Mwenyekiti, Tumeamua kurejesha kada ya askari ardhi (Land Rangers) katika Halmashauri zetu ili kudhibiti uvamizi wa maeneo ya wazi na ujenzi holela na kwa kuanzia tumeanza na Jiji la Dar es Salaam. Na kadri bajeti itakavyoruhusu tutaendelea kuajiri na kuwasambaza katika Halmashauri za Miji na Wilaya.
(c) Kutekeleza Programu ya Taifa ya Kurasimisha na Kuzuia Makazi Holela Mijini. Ndugu Mwenyekiti, Mradi wa urasimishaji unatekelezwa kwa lengo la kuboresha maeneo holela mijini na unafanyika katika Majiji ya Dar es Salaam na Mwanza. Katika kutekeleza Mradi huu fedha nyingi zimetengwa katika utekelezaji. Katika hili kuna maswali ya msingi ya kujiuliza: Kwa mfano, leseni zinazotolewa zimesaidia kwa kiwango gani wananchi kupunguza umaskini wa kipato au kuboresha mazingira ya makazi? Kwa kiwango gani urasimishaji umepunguza uanzishwaji wa maeneo mapya yaliyojengwa kiholela? Majadiliano yetu yajikite katika kubuni njia ya kupunguza gharama za mradi na kuanisha njia mbadala ya kuzuia makazi holela.
Ndugu Mwenyekiti, Mabadiliko katika utendaji na fikra miongoni mwa watumishi katika sekta ya ardhi: Ningependa kuona mkutano huu unakuja na mapendekezo muhimu kuhusu yafuatayo:-
(i) Njia za kuepuka uzalishaji wa migorogoro mipya ya ardhi;
(ii) Mbinu mpya za kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi bila kuathiri waliopo hususani wanaomiliki ardhi. Mjadili ni kwa namna gani wananchi hawatakuwa maskini zaidi kutokana na utekelezaji wa mipango yetu.
(iii) Mbinu bora za kutathimini na kulipa fidia, kuangalia viwango vya fidia.
(iv) Njia nzuri ya kuweka kumbukumbu za ardhi
(v) Mbinu za kuandaa na kuteleza miradi
(vi) Mbinu za kuwezesha wananchi wengi kumiliki nyumba badala kumiliki viwanja tupu au vyenye nyumba ambazo hazitumiki kwa kuwa ujenzi haujakamilika. Hapana budi kutafakari namna ya kubadili mtazamo wa kila mtu kutafuta kiwanja ili ajenge nyumba. Utaratibu huu ndiyo mama wa migogoro ya ardhi nchini. Wanaotafuta ardhi wengi wao wanahitaji nyumba. Wekeni mazingira yatakayofanya watu wanaohitaji nyumba wasilazimike kutafuta ardhi.
Mkutano huu uwe mwanzo wa kubadilika kifikra miongoni mwa watendaji katika sekta ya ardhi ili kutoa huduma bora za ardhi. Ili kufanikiwa lengo hili ni lazima kufanya kazi kama timu kati ya Wizara na Halmashauri za Miji na Wilaya. Huu si wakati wa kila mtu kucheza kivyake. Kila mmoja azielewe changamoto zake na ajiwekee mikakati ya kuziondoa. Lakini afanye hivyo kwa kushirikina na wengine. Ajue hatua gani itakwamisha au itamsaidia mwingine kutekeleza majukumu yake.
Ndugu Mwenyekiti, Ninaamini mkutano huu utakuwa ni dira ya kubaini vema tulikotoka, tulipo na tunakoelekea. Tukifanikiwa hilo tutaweza kujipanga tufikie kiwango cha huduma ambacho kitajenga taswira nzuri ya sekta ya ardhi katika kipindi kijacho.
Ninapenda kumshukuru pia Katibu Mkuu wa Wizara kwa kuwezesha mkutano huu kufanyika. Ni gharama kubwa kuandaa mkutano mkubwa kama huu hasa katika mazingira ya ufinyu wa bajeti uliopo. Ninaamini kwa dhati kuwa matokeo ya mkutano huu yataleta ‘value for money’. Yapo mengi ambayo tusingeyapata au kuyafahamu kama mkutano huu usingeitishwa. Ninaamini kuwa mkutano utatujenga na kuwa timu. Kwa pamoja tutaweza kushinda changamoto zetu. Naomba kila mmoja ajiangalie kama amekuwa kikwazo kwa timu, ajirekebishe. Kama anasaidia timu aongeze juhudi, na awahimize wanaoonekana kulegalega katika utekelezaji wa majukumu.
Ninawashukuru tena kwa kufika kwenu katika mkutano huu. Mijadala itakayofanyika iwe ya mafanikio. Michango yenu iwe ya ukweli na uaminifu. Ninaamini maazimio yenu yatakuwa yanaongeza umoja na ubora wa huduma zetu kwa wananchi kwa kuzingatia, ueledi, uaminifu, na kuzingatia sheria na kanuni.
Sasa natangaza kuwa Mkutano Mkuu wa Sekta ya Ardhi wa Mwaka 2011 umefunguliwa rasmi. Karibuni Sana.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.