Utangulizi
Mji mpya ni mji uliopangwa kwa uangalifu kutoka mwanzo kwa kutumia dhana maalum za kimipangomiji katika eneo ambalo ama halijaendelezwa au limeendelezwa. Jiji la Dar es Salaam ni kitovu kikuu cha shughuli mbalimbali za kiuchumi, kijamii, kibiashara, kitamaduni na diplomasia nchini Tanzania. Aidha, Jiji hili ni kituo kikubwa cha kitaifa na kimataifa chenye mawasiliano ya anga, nchi kavu na majini. Hali hii inawezesha shughuli za biashara, makazi, taasisi (za kitaifa na kimataifa) hoteli, burudani, usafiri na usafirishaji kushamiri ingawaje bado kuna mahitaji makubwa ya huduma hizo, ili kukidhi shughuli muhimu za kimji kufanyika kwa ufanisi na katika hali ya ustawi.
Uzingatiaji wa Maslahi ya Wananchi
1. Uzingatiaji wa maslahi ya wananchi utakuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 Fungu la 3 kijifungu (g) cha fidia kwa bei ya soko.
2. Suala la kuingia ubia litazingatia maendelezo yaliyopangwa katika eneo na matumizi ya ardhi yaliyokuwepo wakati mchakato wa Mpango wa Mji Mpya ulipoanza. Utaratibu wa kuwezeshwa utaratibiwa na kusimamiwa na Serikali.
3. Upewaji wa eneo mbadala ama eneo la kwenye jengo la mbadala utazingatia makubaliano yatakayoratibiwa na Serikali kwa kuzingatia sheria zilizopo na utaratibu utakaowekwa.
4. Aidha Serikali itakuwa inafanya maboresho ya viwango vya bei ya ardhi na mimea/mazao kwa kadiri ya soko linavyobadilika.
5. Maandalizi ya Mpango Kabambe yatakamilika mwezi Juni 2010, na hatua zitakazoendelea zitawekwa bayana kupitia matamko ya Serikali na mikutano mbalimbali ya wadau
Dhana ya Uendelezaji Mji Mpya Kigamboni
Dhana ya Mji Mpya Kigamboni ni mojawapo ya juhudi za Serikali katika kukabiliana na changamoto za miji yetu hapa nchini. Utekelezaji wa dhana hii umeshaanza kwa Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa ndilo linaloongoza kwa ukuaji wa idadi ya watu ambayo inakadiriwa kuwa asilimia 7.3 kwa mwaka. Inakadiriwa kuwa Jiji lina watu wapatao milioni 4, idadi inayolifanya Jiji la Dar Es Salaam sasa kuwa “Metropolitan City” na lina Manispaa tatu (3) za Ilala,Temeke na Kinondoni. Kuna eneo la kati au kitovu (Central Business District-CBD) kimoja tu chenye msongamano wa shughuli nyingi za huduma. Kutokana na hali hiyo, upo umuhimu wa kuwa na eneo lingine la kuendeleza utoaji huduma zinazohitajika za kimji ambazo kwa sasa zinakosekana katika kitovu kilichopo. Huduma hizo zinahitajika ili kukidhi mahitaji ya idadi ya sasa na baadaye ya wakazi, wageni wa ndani na wale wanaotoka nje ya jiji.
Katika kufanikisha mpango huo, yafuatayo yametekelezwa:
1. Kutayarisha andiko/mada kuhusu uendelezaji wa Mji Mpya Kigamboni mwishoni mwa mwaka 2007
2. Warsha ya kuelimisha wadau mbalimbali ili kupata maoni yao kuhusu dhana ya Mji Mpya Kigamboni iliyofanyika tarehe 17 Aprili 2008.
3. Kubainisha eneo la mpango katika Mchoro wa Mipango Miji namba 1/38/5008 wa tarehe 9.6.2008. Eneo hilo lina Kata 4 za Kigamboni, Mjimwema, Vijibweni, Kibada na sehemu ndogo ya Kata ya Somangila, katika mitaa ya Kizani na Mbwamaji. Eneo la Mpango lina ukubwa wa Hekta 6,000 ambalo litahusisha pia visiwa vya Kendwa na Sinda (Inner and Outer Sinda).
4. Eneo la mpango lilitangazwa kisheria, kwa Tangazo la Serikali (GN) namba 229 la tarehe 24/10/2008
5. Tamko la Serikali la tarehe 30/10/2008 lililenga kuuhabarisha umma kuhusu mpango na kusimamisha uendelezaji wowote katika eneo la Mpango kwa miaka miwili kwa mujibu wa sheria ya mipangomiji namba 8 ya 2007 kifungu cha 24 liltolewa.
6.Kufuatia umuhimu wa visiwa vitatu vilivyoko kwenye eneo la mpango paliongezwa sehemu ya kata ya Somangila, mitaa ya Kizani na Mbwamaji. Tamko la Serikali kuhusu eneo la nyongeza lilitolewa tarehe 17/09/2009.
7. Aidha uendelezaji wa aina yoyote unaoendelea katika eneo la Mpango baada ya Tangazo na Tamko la Serikali utakuwa ni uvunjaji wa sheria kwa mujibu wa Sheria ya Mipangomiji namba 8 ya mwaka 2007 kifungu cha 24.
8. Ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu nia ya Serikali ya kupanga eneo husika viongozi na wananchi katika ngazi zote za Mkoa, Wilaya, Kata na Mitaa walielimishwa kuanzia Desemba 2008 hadi Machi 2009.
9. Ofisi za Mpango wa Uendelezaji Mji Mpya Kigamboni zimefunguliwa kwenye ofisi ya Afisa Tarafa ya Kigamboni/Polisi Wilaya ya Kigamboni na sasa shughuli za Mji Mpya zinafanyika hapo siku za Jumatatu na Jumatano saa 3 asubuhi hadi 9.30 alasiri.
Upangaji na Uendelezaji Miji Tanzania
Serikali kwa kutumia mamlaka zake zilizoainishwa kisheria katika kutekeleza majukumu ya upangaji na kusimamia uendelezaji wa miji nchini inazingatia taratibu, viwango na miongozo ya kisheria. Upangaji na uendelezaji wa miji Tanzania ni jukumu linalotekelezwa kwa mujibu wa Sera na Sheria za nchi. Sheria kuu inayohusika ni Sheria ya Mipangomiji namba nane (8) ya mwaka 2007, ambayo inaelezea taratibu na viwango vinavyotumika katika kupanga na kuendeleza maeneo yote yaliyoainishwa kuwa miji.
Sera na Sheria zinazotumika katika upangaji na uendelezaji wa miji ni kama ifuatavyo:
Sera ya Ardhi ya mwaka 1995
Sera ya Makazi ya mwaka 2000
Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999
Kutokana na Sera na Sheria zilizotajwa hapo juu Serikali hutangaza maeneo yanayofaa kuwa miji kwa kutumia gazeti la Serikali na hutoa maelezo au matamko na matangazo kuhusiana na upangaji tajwa hapo juu. Kwa Jiji la Dar es Salaam zoezi hili lilifanyika mwaka 1993 kwa Tangazo la Serikali namba 231 kwa kutangaza eneo lote la Jiji la Dar es Salaam lenye kilomita za mraba zipatazo 1800 kuwa ni eneo la mpango. Kwa kuzingatia Tangazo hilo Serikali imekuwa na utaratibu wa upangaji wa maeneo kutegemeana na uwezo na rasilimali zilizopo.Utaratibu huu unazingatia pia Mipango iliyopo ya kuendeleza Jiji la Dar es Salaam, kama Mpango Kabambe wa Jiji la Dar es Salaam wa mwaka 1979 na Mpango Mkakati wa Dar es Salaam wa mwaka 1992 ambao ulizingatia maudhui ya Mpango Kabambe wa 1979. Mipango mingine ni pamoja na Mpango wa Uendelezaji Upya eneo la Kati la Jiji la Dar es Salaam wa mwaka 2001, Mpango wa Uendelezaji Upya eneo la Kariakoo wa mwaka 2002 na Mpango wa Uendelezaji Upya eneo la Kurasini wa mwaka 2002. Mfumo wa upangaji wa maeneo ya miji nchini unazingatia ushiriki na ushirikishwaji wa sekta binafsi (Public Private Partnership – PPP) pamoja na wadau husika.
Kwa maelezo zaidi bonyesa hapa